Biblia inatuonyesha namna ambavyo Bwana Mungu anataka watu wake wawe hodari katika kufanya yale aliyowaamuru wayafanye; hakuna haja ya kuogopa kwa sababu Roho Yake ipo kati ya watu Wake.
Kama wewe ni mwaminini basi huna haja ya kuogopa kwa sababu yale aliyosema nao wakati ule bado yanakuhusu wewe hata leo hii kwa sababu kama mwamini bado Roho Mtakatifu yuko ndani yako. Ukiwa hodari kufanya kazi ya Bwana ndipo utaona utukufu wa mwisho unakuwa mkuu kuliko utukufu wa kwanza.
Sikiliza fundisho hili, utaimarika.
Mtu asiyeogopa ni jasiri, na mtu jasiri ana kauli tofauti na mtu mwoga. Waoga hukimbia wasipofuatiwa na mtu yeyote bali mwenye haki ni jasiri kama simba. Mwenye haki, haki ipatikanayo kwa imani katika Kristo Yesu, ni mtu jasiri katika Bwana na anapaswa kujua kwamba Bwana anategemea kauli yake iwe tofauti na mwoga asiye haki. Kama wewe ni mwenye haki katika Bwana kwa imani ni vema ukajifunza namna kauli yako inapaswa kuwa. Jifunze kuwa na kauli ya mtu jasiri.
Mtu asiyeogopa ni jasiri, na mtu jasiri ana kauli tofauti na mtu mwoga. Waoga hukimbia wasipofuatiwa na mtu yeyote bali mwenye haki ni jasiri kama simba. Mwenye haki, haki ipatikanayo kwa imani katika Kristo Yesu, ni mtu jasiri katika Bwana na anapaswa kujua kwamba Bwana anategemea kauli yake iwe tofauti na mwoga asiye haki. Kama wewe ni mwenye haki katika Bwana kwa imani ni vema ukajifunza namna kauli yako inapaswa kuwa. Hii ni trailer ya somo la kujifunza kuwa na kauli ya mtu jasiri.
Kutoogopa ni suala la imani kwa sababu inakupasa kusimama na maandiko kwa imani kwamba yuko Mungu anayakuzungukia pande zote na tena anayeangalia kwamba ufikie mwisho mwema. Na pia kwa sababu woga ni udhihirisho wa kutoamini au kuwa na imani haba hivyo haikwepeki kwamba mambo yanayoathiri imani yako yanagusa moja kwa moja kuogopa au kutoogopa kwako. Katika episode hii tunaangalia mambo manne yanayoathiri imani ili kukuwezesha kuikuza imani yako uweze kuwa jasiri, usiyeogopa, kwa sababu Biblia inasema usiogope.
Sasa hivi kuna vita vinapiganwa kati ya Urusi na Ukraine, taifa dhidi ya taifa, na bado chokochoko za vita kusambaa ni kubwa. Huku Afrika vita vya wenyewe kwa wenyewe zimezoeleka. Lakini bado tunafahamu kwamba majaribio ya silaha kali na ripoti za gunduzi mbalimbali za namna za kupigana vita na kuua mamilioni ya watu kwa muda mfupi zinavyotisha wengi. Kuhusu siku hizi za mwisho, Yesu alisema "msiogope mtakaposikia matetesi ya vita". Karibu tujifunze...
Katika nyakati hizi tulizopo sio kitu kigeni masikioni kusikia mtoto kabakwa au kanajisiwa, kauawa na dada wa kazi au kaibwa. Yaani kesi ni chungu nzima. Mambo ni magumu kiasi kwamba wazazi wanaishi kwa hofu juu ya watoto wao. Kama wewe ni mzazi na unamwamini Mungu Aliye hai katika Kristo Yesu basi huna haja ya kuogopa kwa sababu ya Jina hili la fahari na lenye kutisha. Watoto hao aliokupa Bwana wanalindwa na Yeye mwenyewe.
Moja ya jambo litakalokufanya usiogope ni kumcha Bwana. Lakini si tu kutoogopa, Kumcha Bwana kunaleta mambo mengi ya baraka maishani mwako. Lakini hata kumcha Bwana maana yake nini? Haya ndiyo tunayojifunza katika episode hii.
Biblia Inasema Usiogope; usiogope nini? Yako mengi ambayo watu wanayaogopa lakini Biblia inasema usiyaogope. Katika episode hii tunaangalia mambo 7 ya kutoogopa ili kupiga hatua katika imani.
Katika maisha ya imani Shetani hupigana vita ili kututoa katika ujasiri tulionao katika Kristo Yesu. Na adui hufanikiwa katika hili pale anapoweza kutujaza dhamiri ya hatia ndani yetu kwamba sisi ni wakosa na hatuna haki mbele za Mungu. Wakristo wengi wanaishi katika dhamiri ya hatia au wataingia kwenye huo mtego hivi karibuni kwa sababu wameshapelekwa kwenye kona ya kuamini kwamba haki yao inatokana na matendo yao mazuri, yaani hawajavunja sheria au torati. Haki yetu haitokani na sheria bali imani na tena tunalo ondoleo la dhambi. Hati iliyokuwa na mashtaka dhidi yako iligongomewa msalabani pale alipokufa Mwokozi wa ulimwengu. Huna hatia! Sikiliza somo hili.
Mara nyingine tunakuwa na imani ya kuanza kitu au kupokea uponyaji lakini baada ya muda kidogo uponyaji unapeperuka au kile tulichokianza kinakwama. Tunakuwa kama Petro ambaye alianza kutembea juu ya maji halafu akaona upepo mkali akaogopa na kuanza kuzama. Tunaacha kuangalia chanzo cha imani yetu, yaani Kristo Yesu, na kuangalia mazingira. Kumbuka mwenye haki ataishi kwa imani si kwa kuona.
Katika maisha unapokuwa unafanya mapenzi ya Mungu, wale wanaoinuka dhidi yako yaani watesi wako na kwa sababu unafanya mapenzi ya Mungu basi watesi wako wanakuwa kinyume na Mungu. Kama uko katika mapenzi ya Mungu na unakutana na watesi, jipe moyo, maandiko yanasema watesi wako wataanguka.
Tumepewa mamlaka ya kukanyaga simba na nyoka, naam, mwanasimba na joka tunapaswa kuwaseta kwa miguu. Ukifuatilia hili "joka" ambalo Mkristo umepewa mamlaka ya kulikanyaga utafahamu kwamba ni lile joka, yaani Shetani au Ibilisi kwa jina. Kwa mamlaka uliyonayo siyo tu kwa vibaraka wa shetani bali hata kwa shetani mwenyewe. Ndiyo maana maandiko yanasema mpingeni Shetani naye atawakimbia. Kama baba yao anawakimbia itakuwaje kwa wanae, yaani wachawi!? Kama umeokoka na unajua mamlaka na nguvu ulizonazo, wewe ni tishio kwa nguvu za giza. Sikiliza somo hili fupi ukawafundishe na wengine.