Ripoti mpya ya pamoja kutoka mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa lile la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) na la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) inaonya kwamba uhaba mkubwa wa chakula unazidi kuongezeka katika maeneo 16 yenye njaa duniani, hali inayoweza kusababisha mamilioni zaidi ya watu kukumbwa na njaa kali au hatari ya kufikia kiwango cha baa la njaa. Anold Kayanda na maelezo zaidi.
Ripoti mpya ya pamoja kutoka mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa lile la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) na la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) inaonya kwamba uhaba mkubwa wa chakula unazidi kuongezeka katika maeneo 16 yenye njaa duniani, hali inayoweza kusababisha mamilioni zaidi ya watu kukumbwa na njaa kali au hatari ya kufikia kiwango cha baa la njaa. Anold Kayanda na maelezo zaidi.
Mpango wa Ufadhili Wajasiriamali Wanawake, (We-Fi) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia na wadu umewezesha biashara kukwamuka nchini Tanzania baada ya janga la COVID-19, hatua ambayo imeinua pia jamii nzima na si wajasiriamali wanawake peke yao. Simulizi hii ya Assumpta Massoi inamulika mjasiriamali mwanamke Haika Lawere anayemiliki hoteli ya Mbezi Garden jijini Dar Es Salaam ambako ni jiji kuu la biashara la taifa hilo la Afrika.
Kilimo ni moja ya sekta muhimu za kiuchumi nchini Nigeria, kikiajiri zaidi ya theluthi moja ya watu wote nchini humo. Lakini hali ya hewa isiyotabirika imefanya kilimo kuwa shughuli yenye mashaka makubwa — ukame, mafuriko na mvua zisizo na mpangilio zimekuwa tishio kubwa kwa wakulima, ambapo kilio chao kimesikiwa na Benki ya Dunia iliyokuja na suluhisho kwa kuanzisha mradi wa kilimo cha umwagiliaji. Selina Jerobon ana taarifa zaidi.
Hii leo jaridani tunaangazia hali ya haki za binadamu nchini Sudan, Mpango wa Ufadhili Wajasiriamali Wanawake, (We-Fi) nchini Tanzania, na kilimo ni moja ya sekta muhimu za kiuchumi nchini Nigeria.
Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, karibu!
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imetoa tamko juu ya wasiwasi mkubwa kufuatia ripoti mpya kutoka El-Fasher, jimboni Darfur Kaskazini, nchini Sudan, zikieleza kuwepo kwa mauaji ya halaiki, ubakaji, na uhalifu mwingine unaodaiwa kufanywa wakati wa mashambulizi ya Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF). Taarifa zaidi na Sheilah Jepngetich.
Dunia leo ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Majiji, majiji ya kisasa pamoja na kukumbatia teknolojia yametakiwa kuhakikisha yanazingatia zaidi watu ili wengine wasiachwe nyuma au kutengwa na maendeleo hayo. Anold Kayanda na maelezo zaidi.
Mpango wa “Chaguo Langu, Haki Yangu” nchini Tanzania ni jitihada thabiti zinazolenga kuwawezesha wanawake na wasichana kuishi maisha huru dhidi ya ukatili na vitendo hatarishi. Kwa ufadhili wa Serikali ya Finland, Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la IPS, linafanya mabadiliko halisi katika jamii. Sheilah Jepngetich anafafanua zaidi.
Hii leo jaridani tunaangazia Siku ya Kimataifa ya Majiji, vifo na majeruhi vilivyotokea katika maandamano yanayohusiana na uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Tanzania na uwezeshaji wa wanawake nchini huko huko Tanzania.
Mwenyeji wako ni Assumpta Massoi, karibu!
Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu imeeleza wasiwasi mkubwa kufuatia vifo na majeruhi vilivyotokea katika maandamano yanayohusiana na uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Tanzania tarehe 29 mwezi huu wa Oktoba. Selina Jerobon na taarifa zaidi.
Katika kujifunza lugha ya Kiswahili hii leo, mtaalam wetu Onni Sigalla, Mhariri mwandamizi wa Baraza la Kiswahili la Taifa nchini Tanzania, BAKITA. Anafafanua maana za neno "SUMIA."
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina ambayo Bi. Lucy Githinji, mkazi wa jimbo la New Jersey nchini Marekani amezungumza na idhaa hii baada ya matembezi ya hiari kwa ajili ya kuhamasisha jamii kuhusu saratani ya titi, akisema hakika dawa zinafanya kazi.
Mwenyeji wako ni Assumpta Massoi, karibu!
Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, WHO, limeongoza uhamishwaji wa wagonjwa kutoka Gaza eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israeli, ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuanza kwa awamu mpya ya kusitishwa kwa mapigano kwenye ukanda huo.
Katika muda wa siku mbili, wagonjwa 41 waliokuwa katika hali mbaya pamoja na familia zao 145 wamehamishwa kutoka eneo la mgogoro, kuelekea Afrika Kusini, Uswisi na kwingineko, huku maelfu zaidi wakiendelea kusubiri matibabu ya dharura.
Katika hospital iliyojengwa kwa mahema katika eneo la AL-MAWASI, RAFAH kwenye Ukanda wa Gaza wagonjwa wakihudumiwa kila kona watoto kwa wakubwa Miongoni mwao ni Ibrahim Abu Ashiba, mkurugenzi wa filamu ambaye maisha yake yamebadilika ghafla. Anakumbuka wakati alipojeruhiwa.
Anasema, "Nilipigwa risasi mara kadhaa, mara moja kwenye kifua, mara moja kwenye bega, mara mbili mkononi. Risasi hizo mbili zilikata mishipa ya neva ya mkono wangu. Sasa siwezi kushika kamera wala kunyoosha mkono wangu kawaida. Ghafla, maisha yangu yote yalisimama."
Safari ya kupona kwa Ibrahim inaanzia Afrika Kusini, ambapo amekubaliwa kwenda kupokea matibabu maalum ambapo anasema "Maisha yangu yote yalikuwa yamesimama baada ya kujeruhiwa hadi waliponipigia simu na kunijulishakwamba nitasafiri kwenda Afrika Kusini kwa matibabu. Ilionekana kama nimezaliwa upya."
Mgonjwa mwingine katika hospitali hii ni, Maria Al-Shaer, alijeruhiwa vibaya katika mashambulizi yaliyokuwa yakiendelea Gaza, huku akipoteza ndugu zake. Mama yake, Raghda Ahmed Al Shaer, anaelezea mateso hayo.
"Maria amepoteza baba yake na ndugu zake wote. Alijeruhiwa na kuvunjika mguu, mifupa na kupoteza nyama. Anahitaji upasuaji wa kuwekewa viungo bandia. Maisha yake yamegeuka, hawezi kutembea, na hali yake ya kisaikolojia imeathirika sana."
Uhamishwaji huu umeratibiwa na Shirikisho la Chama cha Msalaba Mwekundu Palestina, kwa msaada wa WHO. Dkt. Luca Pigozzi, Mratibu wa Timu ya Dharura ya WHO, anafafanua umuhimu wake.
"Huu ni uhamishaji wa kwanza wa matibabu tangu kusitishwa kwa mapigano Oktoba 10. Tumejizatiti kuongeza uwezo wetu kusaidia na kuratibu uhamishaji kwa ajili ya matibabu, kwa ushirikiano wa karibu na Shirikisho la chama cha Msalaba Mwekundu la Palestina."
Raghda anaeleza matumaini kwa ajili ya binti yake wanapohama kwenda Uswisi. "Wametupigia kutuarifu kwamba Maria amekubaliwa kusafiri kwenda Uswisi kwa matibabu. Tumefurahi sana kwamba atatembea tena, na hali yake ya kisaikolojia itaboreka. Atarudi kuwa Maria wa kawaida kama tuliyemjua."
WHO inasisitiza kuwa wagonjwa takriban 15,000 bado wanangojea idhini ya kupata matibabu nje ya Gaza na inatoa wito kwa nchi zote kufungua milango yote za dharura kwa ajili ya uokoaji wa wagonjwa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameonesha wasiwasi mkubwa wakati huu Kimbunga Melissa kikiwa miongoni mwa vimbunga vyenye nguvu zaidi kuwahi kurekodiwa katika Bahari ya Atlantiki kinaendelea kusababisha uharibifu mkubwa katika eneo la Karibea.
Kupitia taarifa yake iliyotolewa leo mjini New York Marekani na msemaji wake, Katibu Mkuu amesema kimbunga hicho kimeacha madhara makubwa nchini Jamaica, Cuba na Bahamas huku mafuriko makubwa yakiripotiwa pia nchini Haiti na Jamhuri ya Dominika.
Taarifa hiyo imemnukuu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwamba “ana wasiwasi mkubwa” na anashikamana na serikali pamoja na wananchi walioathiriwa vibaya na Kimbunga Melissa.”
Katibu Mkuu pia “Amewapa pole familia zote za waliopoteza wapendwa wao katika kimbunga hicho na anawatakia majeruhi wote ahueni ya haraka.”
Umoja wa Mataifa umeanza kutoa msaada wa dharura, huku timu zake zikiwa tayari mashinani kusaidia kutathmini madhara na kusaidia juhudi za kitaifa. Pia, umetoa dola milioni nne kwa Haiti na vile vile dola milione nne kwa Cuba kutoka Mfuko wake wa Dharura (CERF) ili kusaidia jamii kujiandaa na kupunguza madhara ya kimbunga hicho.
Taarifa hiyo imesema Umoja wa Mataifa uko tayari “kutuma wahudumu wa ziada kwa muda mfupi na kuzindua maombi ya misaada ya dharura kukabiliana na mahitaji ya kibinadamu yatakayosababishwa na kimbunga hicho.”
Kimbunga Melissa ni miongoni mwa vimbunga vyenye nguvu zaidi kuwahi kuikumba Karibea, na kinatishia maisha ya mamilioni ya watu kutokana na mafuriko, uharibifu na watu kufurushwa katika makazi yao.
Leo jaridani tunamulika kimbunga Melissa huko Karibea, uhamishaji wagonjwa kutoka Gaza kwenda nchi za nje kupata huduma za kigeni na hali tete kwa watoto nchini Sudan. Mwenyeji wako ni Assumpta Massoi.
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayoangazia mradi wa TANZIE huko Chuo Kikuu Mzumbe, mkoani Morogoro, mashariki mwa Tanzania, unaolenga kusongesha Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs. Pia tunakuletea habari kwa ufupi na uchambuzi wa neno la wiki.
Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, karibu!
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ametoa wito kwa dunia na mataifa wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kusini-Mashariki mwa Asia, ASEAN kuchukua hatua za haraka kumaliza machafuko ya muda mrefu nchini Myanmar, akisisitiza kuwa mgogoro huo si tishio kwa watu wa Myanmar pekee bali pia kwa amani na usalama wa kanda nzima ya Asia ya Kusini Mashariki. Assumpta Massoi na maelezo zaidi.
Katika kaunti ya Mombasa nchini Kenya, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kwa kushirikiana na wa Mastercard Foundation na Serikali ya Kaunti ya Mombasa, imechukua hatua za kukabiliana na mlipuko wa MPOX kwa kutoa huduma muhimu za afya na WASH kwa wagonjwa na waliopona, ikiwa ni pamoja na vifaa vya kujikinga (PPEs), vituo vya kusafisha mikono na ujumbe wa mabadiliko ya tabia za kijamii. Sheilah Jepngetich na taarifa zaidi
Hii leo jaridani tunaangazia machafuko ya muda mrefu nchini Myanmar, hali ya kibinadamu nchini Sudan kufuatia ripoti za vifo vya raia na wimbi la wakimbizi wa ndani, na masuala ya afya nchini Kenya.
Mwenyeji wako ni Flora Nducha, karibu!
Ofisi ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imeelezea wasiwasi mkubwa kufuatia ripoti za vifo vya raia na wimbi la wakimbizi wa ndani, kufuatia kuendelea kwa mapigano makali katika mji wa El Fasher, huko Darfur Kaskazini nchini Sudan. Tupate tarifa zaidi kutoka kwa Leah Mushi
Msikilizaji, bila shaka umeyasikia mengi kuhusu Umoja wa Mataifa, lakini Umoja wa Mataifa ni nini hasa? Japo kwa ufupi, Anold Kayanda anakufahamisha akianza na historia.