
Wakati watahiniwa zaidi ya milioni moja wa elimu ya msingi Tanzania Bara wakiwa wanasubiri hatma yao, baada ya kumaliza mitihani yao jana Septemba 14, 2023, utoshelevu wa walimu katika ngazi hiyo muhimu ya elimu kwa shule za Serikali umeendelea kuwa kitendawili
Kitabu cha hali ya uchumi cha mwaka 2022, kinabainisha kuwa mpaka Disemba mwaka 2022 kulikuwa na jumla ya wanafunzi milioni 10.8 katika shule za msingi za Serikali Tanzania, huku idadi ya walimu katika shule za Serikali ikiwa 173,276.
Hii ni sawa na kusema idadi ya wanafunzi waliopo ni mara 62 zaidi ya idadi ya walimu na hivyo kwa wastani mwalimu mmoja hufundisha darasa lenye wanafunzi 63 kwa wakati mmoja uwiano ambao uko juu ya kiwango kinachotakiwa cha wanafunzi 45 kwa darasa.
Aidha, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) inataja Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma kuwa ndio wilaya ambayo mwalimu mmoja hufundisha darasa lenye wanafunzi wengi zaidi wanaofika 103.
Wilaya ya Muleba iliyopo mkoani Kagera ndiyo wilaya pekee iliyofanikiwa kufikia uwiano stahiki kwa wanafunzi 45 kufundishwa na mwalimu mmoja kwa darasa mwaka 2021.
Wadau wa elimu nchini Tanzania, wanatoa maoni yao juu ya namna upungufu wa walimu shule za msingi unavyoathiri sekta ya elimu nchini.
Karibu.