
Huenda wachimbaji wadogo wa madini Tanzania wakaepukana na athari za afya pamoja na uchafuzi wa mazingira ikiwa wataasili matumizi ya bidhaa mpya ya kusafishia madini (Activated carbon) inayozalishwa nchini.
Bidhaa hiyo inayotengenezwa kwa kutumia vifuu vya nazi itachochea uzalishaji wa madini na kuongeza mchango wa sekta hiyo kwenye pato la taifa kwa kuwa itapatikana kwa urahisi jambo litakaloongeza kasi katika shughuli za uchenjuaji huku mazingira na wachimbaji wakwa salama.
Upatikanaji wa bidhaa hiyo mbadala wa zebaki katika shughuli za uchechuaji itakuwa mkombozi kwa wachimbaji pamoja na jamii ambayo inaweza kuathirika kwa kwa kuvuta hewa, kula chakula au maji yaliyo na sumu ya zebaki.
Shirika la Afya Duniani (WHO), linabainisha kuwa athari za kiafya zitokanazo na zebaki ni pamoja na kuharibiwa kwa mifumo ya neva, kuharibiwa kwa mfumo wa upumuaji, mmeng’enyo, mifumo ya kinga, figo, mapafu na wakati mwingine husababisha kifo.
WHO wamesisitiza kuwa sumu hiyo inaweza kusababisha magonjwa katika mfumo wa fahamu ikiwemo kifafa, kupoteza uwezo wa kuona au kusikia, udumavu pamoja na kupoteza kumbukumbu
Mpango Kazi wa Taifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki 2020/25 unabainisha kuwa zebaki ni miongoni mwa kemikali hatarishi inayosababisha athari kwa afya ya binadamu na mazingira duniani