
Nishati ya kupikia ni miongoni mwa mahitaji muhimu ya binadamu duniani kote, hiyo ndio huwezesha mapishi ya aina mbalimbali za vyakula tunavyokula ili kuimarisha afya na kuwezesha utendaji wa shughuli za kila siku.
Watu wengi wanatambua gesi, mkaa, umeme, mafuta pamoja na kuni kama ndio vyanzo vya nishati ya kupikia kwa kuwa ndio ambavyo vinatumika kwa kiasi kikubwa kwa sasa huku jitihada nyingi zikielekezwa kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Hata hivyo, jijini Dar es Salaam kuna ubunifu mpya wa nishati ya kupikia inayotumia mawe, ambapo inatajwa kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za kupikia kwa gesi, umeme, mkaa au nishati nyingine.
Ndiyo! Ubunifu, udadisi pamoja na uthubutu umewezesha ugunduzi huu ambapo sasa mawe yanayopatikana kwa urahisi katika maeneo mengi nchini Tanzania yanaweza kutumika kama chanzo cha nishati ya kupikia.
Raymond James (25) maarufu kama Mr Majiko, ndiye mbunifu wa majiko hayo yanayotumia mawe, umeme kidogo pamoja na chenga za mkaa mbadala zinazotokana na vifuu vya nazi.
Kijana huyo mkazi wa Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam, ameiambia Nukta Habari kuwa kukosa ajira ndio sababu kubwa iliyommchochea kubuni majiko hayo ili aweze kujiingizia kipato kitakachomuwezesha kuendesha maisha.
Katika podcast hii, amezungumza mengi. karibu kumsikiliza