
Mapema Agosti mwaka huu Serikali ya Tanzania ilitangaza kukamata magunia 131 ya bangi, kilo 120 za mbegu za bangi na kuteketeza jumla ya hekari 489 za mashamba ya bangi mkoani Morogoro, katika moja ya operesheni kubwa za kutokomeza dawa za kulevya iliyowahi kufanyika nchini.
Katika operesheni hiyo Kamishna wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Aretas Lyimo anasema wakulima hao wa bangi hufanya uharibifu mkubwa wa mazingira kwa kuchepusha maji pamoja na kukata misitu ili kufanya kilimo cha zao hilo haramu.
Watu 18 walikamatwa katika operesheni hiyo iliyoshika mjadala katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii baada ya mamlaka hiyo kueleza kuwa watuhumiwa hao walikuwa wakifanya kilimo katika mazingira ambayo si rahisi kufikika.
Hili ni miongoni mwa matukio makubwa ya kudhibiti dawa za kulevya ndani ya miaka mitano, jambo linaloashiria kuwa washirika wa dawa hizo hatari kwa afya ya binadamu wanaendelea kuzalisha licha ya jitihada za Serikali na wadau kuzidhibiti.
Mwaka 2021 tani 22.74 za bangi zilikamatwa nchini Tanzania ikiwa ni ongezeko la asilimia 72 ya kiasi kilichokamatwa mwaka 2020.
Aidha, takwimu za uhalifu nchini zilizopo katika kitabu cha hali ya uchumi mwaka 2022 kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonesha mashamba ya bangi yameongezeka takriban mara mbili ndani ya miaka minne kutoka 49 mwaka 2018 hadi kufikia mashamba 87 mwaka 2022.