
Tanzania ni miongoni mwa mataifa ambayo yamebarikiwa vivutio vingi vya utalii ambavyo sio tu vinapendezesha nchi bali ni chanzo kizuri cha mapato hususani fedha za kigeni ambazo hutumika kwa shughuli za maendeleo.
Tovuti ya runinga ya Tanzania Safari Channel ambayo hutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini, inabainisha kuwa Asilimia 40 ya ardhi ya Tanzania imetengwa kwa ajili ya uhifadhi.
Hii inajumuisha hifadhi za Taifa 22, eneo la hifadhi ya Ngorongoro, mapori tengefu, hifadhi za misitu asilia na misitu ya kupandwa, maeneo ya kihistoria pamoja na hifadhi za bahari.
Maeneo yote hayo ndio kitovu kikubwa cha utalii nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa kitabu cha hali ya uchumi kwa mwaka 2022, kinachotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS) hifadhi za taifa ni moja kati ya vivutio vilivyotembelewa zaidi na watalii wa ndani na nje ya nchi.
Mwaka 2022 hifadhi hizo zilitembelewa na jumla ya watalii milioni 1.4 kati yao watalii 787,742 walitoka ndani ya nchi na watalii 697,264 kutoka mataifa mengine yaliyopo nje ya nchi.
Huenda wewe ni miongoni mwa watu wanaofahamu kuhusu uwepo wa hifadhi hizi lakini hujui ni ipi inaongoza kwa ukubwa, inapatikana wapi, na gharama za kufika huko.
Makala hii imeorodhesha hifadhi tano ambazo ndio kubwa zaidi nchini Tanzania pamoja na aina ya vivutio utakavyokutana navyo.